Changamoto Zinazowakumba Vijana katika Tamthilia ya Kitumbua Kimeingia Mchanga
Abstract
Katika ulimwengu wa sasa, kuna mabadiliko chungu nzima yanayoshuhudiwa duniani yanasababishwa na masuala anuwai kama vile maendeleo ya kiteknolojia pamoja na utandarithi yanayoathiri pakubwa maisha ya vijana. Nchini Kenya, vijana wana umuhimu wa kipekee kwani wanatekeleza majukumu muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi. Isitoshe, idadi ya vijana kote ulimwenguni imeendelea kuongezeka kila uchao na imepiku ile ya wazee. Kwa hivyo, ni nyema kujadili changamoto zinazowakabili na kupendekeza hatua za kukabiliana nazo. Lengo la utafiti huu lilikuwa ni kuchanganua changamoto zinazowakumba vijana pamoja na athari zake katika ya tamthilia ya Kitumbua Kimeingia Mchanga ya S.A Mohamed (2000). Mada hii ilichaguliwa kwa misingi kwamba vijana wanakumbwa na changamoto nyingi katika maisha yao zinazowaathiri kwa kiasi cha haja na kutinga juhudi za kuafikia jaala zao. Utafiti huu ulilenga kubainisha changamoto zinazowakumba vijana katika tamthilia hii na kutambua mbinu ambazo vijana hawa wanazua ili kukabiliana nazo. Nadharia ya Uhalisia ilitumika kwa sababu ilionekana kufaa zaidi kuchanganua changamoto zinazowakumba vijana. Hii ni kwa sababu changamoto hizi zina uhalisia mkubwa katika maisha yao. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kuchunguza na kueleza namna changamoto za vijana zinavyojitokeza katika tamthilia ya Kitumbua Kimeingia Mchanga na kisha kubainisha hatua zinazochukuliwa kuzitatua changamoto hizo. Utafiti huu ni wa kimaelezo na kiudhamano kwani ulihusisha kuchanganua matini zinazohusiana na mada husika. Sampuli katika utafiti huu iliteuliwa kimakusudi kwani ndiyo ingempa mtafiti data aliyonuia kuipata. Ni bayana kuwa utafiti huu utaifaa jamii ya wasomi wanaoshughulikia maswala ibuka katika jamii.